![]() |
Benki ya CRDB imeorodhesha rasmi Kijani Bond yake katika Soko la Hisa la Luxembourg (LuxSE), ikiwa benki ya kwanza nchini Tanzania na miongoni mwa chache Kusini mwa Jangwa la Sahara kufanikisha hatua hii. Hatua hii ni ishara ya ujasiri wa Afrika katika kuyakabili mabadiliko ya tabianchi kwa njia za kibunifu na endelevu.
Hafla hiyo ya kihistoria ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Abdulmajid Nsekela, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Luxembourg, Juma Ali Salum, na Afisa Mkuu wa Biashara wa LuxSE Arnaud Delestienne, pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Benki ya CRDB, LuxSE, na Orbit Securities Tanzania.
Kuorodheshwa kwa Kijani Bond katika Soko la Hisa la Luxembourg ni mwanzo wa ushirikiano mpya kati ya Afrika na Ulaya katika kufadhili wa miradi ya kijani. Hatua hii itaiwezesha benki kupanua wigo wake wa kupata mitaji ya kimataifa huku ikiimarisha mchango wake katika kusaidia jitihada za serikali kukuza uchumi wa kijani, hujku ikiiweka Tanzania katika ramani ya vinara wa ufadhili wa miradi endelevu duniani na kuvutia wawekezaji wengi.
Hatifungani ya kijani ilikusanya zaidi ya Shilingi Bilioni 171.8 (sawa na Dola za Marekani Milioni 65.7) ambazo zinaelekezwa katika ufadhili wa miradi ya nishati mbadala, kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, nishati safi ya kupikia, majengo rafiki kwa mazingira, Usafiri wa kijani, maji safi na huduma bora za usafi wa mazingira, pamoja na miradi mingine inayozingatia mabadiliko ya tabia nchi.
